Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kiongozi wa chama cha ODM ambaye pia ni kinara wa muungano wa Cord Raila Odinga amemshtumu Seneta wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kutokana na uhasama baina yake na Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

Raila alitaja tukio ambapo Sonko alimfokea Gavana Joho hadharani, lilitokea katika uwanja wa Shika Adabu eneo la Likoni wakati wa kutoa hati miliki kwa maskwota wa shamba la Waitiki kama la aibu.

Akiongea katika eneo bunge la Nyali kaunti ya Mombasa siku ya Jumatano, Raila alimshtumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kunyamazia swala hilo bila kuongea lolote licha ya kwamba alikuwepo.

“Tuliona Sonko akimtusi gavana wetu mbele ya rais, na badala ya rais kumuonya, yeye alitazama tu bila kuongea,” alisema Raila.

Aidha, alisema kuwa hatua hiyo inaonyesha kwamba rais hawezi akakosoa viongozi katika muungano wake wa Jubilee, hata wanapokiuka maadili.

Wakati huo huo, kiongozi huyo wa upinzani alimsifu Gavana Joho kwa kuonyesha ukakamavu wake wa kutetea chama cha ODM, na kumtaja kama kiongozi anayefahamu siasa halisi.

“Walikuwa wanataka gavana apigie debe Jubilee, lakini ningependa kumshukuru gavana wetu kwa kusimama imara, na kusema wazi kwamba sisi ni ODM na hawawezi kufanya hivyo,” aliongeza Raila.

Matamshi ya Raila yanakuja huku kukiwa na hisia mseto katika kaunti ya Mombasa, kuhusiana na uhasama baina ya Seneta Sonko na Gavana Joho.