Viongozi wa mrengo wa CORD wametangaza kuwa hakutakuwepo na uchaguzi mkuu mwaka ujao iwapo tume ya kusimamia uchaguzi na kuratibu mipaka nchini (IEBC) haitafanyiwa marekebisho.
Akizungumza siku ya Alhamisi, Raila Odinga, alisema kuwa tume hiyo ya uchaguzi ni lazima ivunjwe kabla ya mwaka wa 2017 huku wakisisitiza kuwa tume hiyo haina uwezo wa kuendeleza uchaguzi huru na wenye haki.
Raila alisema haya baada ya wao kupata afueni kufuatia mahakama ya Malindi kutoa uamuzi wa kuagiza serikali kuwacha kuwakandamiza viongozi wa mrengo wa upinzani CORD. Jaji wa mahakama ya juu, Said Chitembwe alitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi baada ya mawakili saba kuandamana na viongozi wa CORD, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula katika mahakama hiyo ya Malindi.
Mawakili hao walijumuisha James Orengo, ambaye ni seneta wa Siaya, Moses Wetangula ambaye ni senator wa Bungoma, Stewart Madzayo ambaye ni seneta wa Kilifi, Amason Kingi ambaye ni gavana wa Kilifi, Anthony Oluoch, Aoko Otieno, Noman Magaya na James Mouko.
Baada ya uamuzi huo wa mahakama, Raila aliuambia umma uliokuwa nje ya mahakama hiyo ya Malindi kuwa kuchaguliwa kwa Willy Mtengo kulikuwa chanzo cha upinzani kushinda uchaguzi mkuu ujao.