Wafuasi wa NASA wakishiriki maandamano dhidi ya IEBC. [Picha/ akelicious.com]
Kiongozi wa NASA Raila Odinga ametakiwa kusitisha maandamano dhidi ya IEBC ikizingatiwa kuwa amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha marudio ya uchaguzi ya urais.Kauli hii imetolewa na katibu mkuu wa KEMNACK Kaunti ya Kwale, Sheikh Hamisi Mwachirumu, aliyesema kuwa maandamano hayo hayana manufaa yoyote.“Haya maandamano yao hayana umuhimu wowote kwa sababu Raila amejiondoa kwenye marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26,” alisema Mwachirumu.Akizungumza na mwandishi huyu, Mwachirumu alisema ni jambo la kushangaza kuwaona wafuasi wa NASA wakishiriki maandamano hayo ilhali kinara wao ametangaza kuwa hatoshiriki katika uchaguzi wa Oktoba 26.“Wafuasi wa NASA wanajisumbua, wanapigwa na jua, hawajui watakula nini ilhali Raila amejiondoa kwenye uchaguzi,” alisema Mwachirumu.Alisema kuwa taifa litaendelea kupata hasara na uchumi kudorora iwapo maandamano hayo yataendelea.“Maandamano yao yanaleta hasara kwa taifa. Biashara zinaathirika na uchumi unazidi kudorora kwa sababu ya watu wachache,” aliongeza.Mwachirumu ameitaka idara ya usalama kutokubali kufanyika kwa maandamano hayo ya NASA na kutaka hatua za nidhamu kuchukuliwa kwa watakaohusika.“Polisi wanapaswa kuwatia mbaroni watakao husika katika maandamano hayo na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao,” alisema Mwachirumu.