Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kiongozi wa muungano wa Cord Raila Odinga alizuru mji wa Mombasa siku ya Jumatano na kutangamana na wafuasi wake mjini humo.

Hafla kubwa iliyomleta eneo hilo ilikuwa ni kuzindua rasmi barabara iliyopewa jina la marehemu mwanawe Fidel Odinga, aliyeaga dunia mapema mwaka wa 2015.

Hafla hiyo ilipata upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya watu nchini, ikiwa ni pamoja na upande wa viongozi wa Jubilee.

Kiongozi huyo wa upinzani alichukua fursa hiyo kuwaelezea Wapwani kuhusu maisha na masaibu aliyopitia marehemu Fidel Odinga wakati wa utoto wake.

Kwanza, alieleza kwamba hakupata nafasi nzuri ya kutangamana na mwanawe huyo wakati akiwa mtoto kwani huo ndio wakati aliokuwa amefungwa gerezani.

“Mara ya kwanza mimi nilipokamatwa na kupelekwa jela, Fidel alikuwa na miaka minane peke yake. Nilipoachiliwa huru, nilimpata akiwa kijana mkubwa wa miaka 15,” alisema Odinga.

Odinga alikumbuka mwaka wa 1982, miaka 34 iliyopita, alipokamatwa na kumuacha Fidel mikononi mwa mamake Bi Idda Odinga katika hali ngumu ya kumlea akiwa peke yake.

“Maisha yalikuwa magumu sana wakati huo. Mama yao alifukuzwa kazi na wakapitia changamoto sana. Lakini hiyo haikuwazuia kuendelea mbele,” aliongeza Odinga.

Umati uliohudhuria ulionekana kuguswa zaidi na historia hiyo aliyokuwa akisimulia, huku baadhi yao wakimtaja kama mwanasiasa mvumilivu.

Odinga alimtaja marehemu Fidel kama kijana aliyekuwa mwenye bidii na mpenda amani, huku akiongeza kuwa uzinduzi wa barabara iliyopewa jina lake sio kwa faida za kisiasa, bali ni kuonyesha vijana wengine nchini umuhimu wa kuwa na bidii katika kila jambo.

Wakati huo huo, aliweka wazi kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa ndio iliyopendekeza barabara hiyo ya Nyali kubadilishwa jina, na kumshukuru Gavana Hassan Joho kwa kuonyesha heshima ya hali juu.

“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa serikali ya Mombasa na Gavana Joho kwa kuonyesha ukarimu wa aina hii,” alisema Odinga.