Mwenyekiti wa chama cha Kanu tawi la Nakuru amemtaja kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kama 'mbwa asiyekuwa na meno'.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wilson Leitich, alisema Raila ni 'mbwa asiyekuwa na meno' na kumuonya kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi dhidi ya kushirikiana naye kisiasa.

Haya yanajiri baada ya ripoti katika baadhi ya vyombo vya habari siku ya Ijumaa kudai kuwa Raila anapanga kumuunga mkono Gideon katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Akizungumza siku ya Jumapili, alipoukaribisha ujumbe wa viongozi wa Kalenjin huko Molo, Leitich alidai kuwa Raila anapanga njama ya kugawanya jamii ya Kalenjin ili kukosesha muungano wa Jubilee kura za bonde la ufa ambazo wataalamu wamesema ni muhimu kwa ushindi wa Jubilee katika uchaguzi wa mwaka 2017.

"Tunafahamu vyema mbinu za Raila. Anatarajia kugawanya jamii ya Kalenjin ili kujifaidi mwenyewe. Tunamtaka Gideon kujitenga na kiongozi huyo,” alisema Leitich.

Raila Odinga anafurahia uungwaji mkono mkubwa katika ngome zake za kisiasa. Hata hivyo, kiongozi huyo hajafanikiwa kuwa rais licha ya kuwania kiti hicho mara kadhaa.

Leitich alisema kuwa jamii ya Kalenjin itazidi kuunga mkono muungano wa Jubilee na Naibu Rais William Ruto bado ndiye kiongozi wa jamii hiyo.