Rais Uhuru Kenyatta ameziagiza idara za usajili wa watu nchini kuhakikisha kuwa vijana waliotimiza umri wa miaka 18 wanapewa vitambulisho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Kenyatta alisema kuwa kila Mkenya ana haki kikatiba ya kupata stakabidhi hiyo ya kitaifa.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa wanahabari siku ya Ijumaa, Rais Kenyatta alisema kuwa stakabadhi hizo muhimu ndizo zinaweza kutumika kubadilisha uongozi wa nchi iwapo Wakenya hawajaridhika na viongozi walio mamlakani.

Rais alisema kuwa kasumba ya hapo awali kuwa raia wa kigeni hutumia fursa hiyo kuingia humu nchini imepigwa marufuku na ukaguzi rasmi utatekelezwa kabla ya mtu kupewa kitambulisho, ili kuzuia kupenya kwa magaidi humu nchini.

Kenyatta alisema kuwa vijana pia wanahaki kikatiba kupiga kura na kuwachagua viongozi walio na nia ya kuwafanyia Maendeleo, na kubadilisha uongozi wa nchi ili kuhakikisha kuwa maswala muhimu yanatekelezewa wananchi.

"Ni lazima vijana waliofikisha umri wa miaka 18 wapewe vitambulisho ili nao pia washiriki moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao. Vijana wana haki kikatiba kupata vitambulisho na kupiga kura,” alisema Rais Kenyatta.

Kauli yake imeungwa mkono na kiongozi wa waliyo wengi katika bunge la kitaifa Adan Duale, huku akiushutumu muungano wa mrengo wa Cord unaotaka kuvunjwa kwa tume ya IEBC.

Rais Kenyatta yuko katika maeneo ya kazkazini wa Kenya akifanya ziara yake ya siku tatu akiambatana na Naibu Rais William Ruto, Waziri wa usalama wa ndani nchini Joseph Nkaissery pamoja na viongozi wengine serikalini.