Shirika la Haki Africa limemtaka Rais Uhuru Kenyatta kutotia saini mswada wa marekebisho ya sheria za uchaguzi uliopitishwa na bunge la kitaifa na lile la Seneti.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa kutoka shirika hilo, Francis Auma, amesema kuwa mswada huo unakiuka katiba na ulipitishwa katika njia ya kutatanisha.

“Mswada huu umepitishwa pasi kuzingatia katiba na maslahi ya mwananchi wa kawaida,” alisema Auma.

Aidha, alisema kuwa huenda kukashuhudiwa machafuko nchini iwapo rais atapitisha sheria hiyo.

“Tuna hofia kuzuka kwa machafuko wakati wa uchaguzi ama hata baada ya uchaguzi, iwapo mswada huo utakuwa sheria,” alisema Auma.

Auma amemtaka rais kurudisha mswada huo kwa bunge kabla ya kutiwa saini ili ufanyiwe majadiliano na vipengee tata kuondolewa.

“Namsihi rais kurudisha mswada huo katika bunge kufanyiwa marekebisho zaidi kabla ya kupitishwa kuwa sheria,” alisema Auma.

Wakati huo huo, amewataka Wakenya kutozua vurugu na kuendelea kuishi kwa amani, ili kuepuka ghasia kama zile za mwaka 2007/2008.

Kauli hii inajiri baada ya bunge la Seneti, likiongozwa na maseneta wa Jubilee kupitisha mswada huo ambao kwa sasa unasubiri kutiwa saini na rais, huku viongozi wa upinzani wakiupiga vikali.

Marekebisho hayo yana ruhusu kutumika kwa mfumo wa zamani wa kupiga kura, pamoja na kutuma matokeo ya uchaguzi.