Mchanganuzi wa maswala ya kiuchumi Johnson Muchiri amemshinikiza Rais Uhuru Kenyatta kulifanyia baraza lake la mawaziri mabadiliko kutokana na kukithiri kwa visa za ufisadi.
Kulingana na Muchiri, iwapo Rais Kenyatta hata chukua hatua hiyo ili kusitisha utumizi mbaya wa fedha za umma zinazofujwa na maafisa wa umma, basi taifa hili litakumbwa na changamoto nyingi za kichumi pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano afisini mwake, Muchiri ambaye pia ni mwanasheria, alisema kwamba asilimia 30 ya maafisa wa umma hushiriki ufisadi nchini na kuchangia serikali kushindwa kuhumudu gharama za nchi.
Muchiri aidha, alisema kwamba kushuhudiwa kwa malumbana ya kisiasa kila uchao kamwe hakutasaidia kuzuia kukithiri kwa kashfa za ufisadi zinazotekelezwa na baadhi ya mawaziri na maafisa wa umma.
Muchiri alimshinikiza Rais Kenyatta kuchukua jukumu hilo la kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri pamoja na kuwatimua kazini maafisa wa umma wanaohusika na ufisadi.
Alipendekeza maafisa wa umma wafisadi kuamriwa kurudisha fedha za umma katika hazina ya serikali kuu ili fedha hizo kutumika katika kuwahudumia Wakenya katika miradi mbalimbali ya kiserikali.
“Tunamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatua za dharura na kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri pamoja na kuwabandua mamlakani maafisa wa umma waliyowafisadi ili taifa hili liwezekumudu gharama za wananchi,” alisema Muchiri.
Kauli ya mwanasheria huyo imejiri huku mchakato mkali wa kushinikizwa kujiuzulu kwa Waziri wa Ugatuzi nchini Ann Waiguru kutokana na kashfa za ufisadi zikizidi kuendelea.