Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano katika Ikulu ya Sagana alifungua rasmi mkutano wa siku mbili unaoleta pamoja maafisa kutoka serikali kuu na wale kutoka serikali za kaunti. 

Mkutano huo wa tano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti unalenga kuangazia ripoti mbalimbali kuhusu hazina ya umma, sheria za kutoza ushuru, mfumo wa mawasiliano IFMIS na usambazaji wa fedha.

Itakumbukwa kuwa magavana walikuwa wamelalama kuhusu changamoto zinazoletwa na mfumo huo wa mawasiliano na teknolojia IFMIS, kuwa unachelewesha ununuzi wa bidhaa. 

Hata hivyo suala hilo linashughulikiwa kupitia kwa kuimarishwa kwa teknolojia na mawasiliano katika kaunti zote. 

Katika mkutano huo vile vile, mamlaka ya ugatuzi itawasilisha ripoti yake kuhusu hatua ambayo serikali imepiga katika kutekeleza ugatuzi kabla ya muda wa utekelezaji huo kuisha. 

Siku ya Alhamisi imetengwa kusherehekea hatua zilizopigwa katika ugatuzi, naibu wa Rais William ruto, mawaziri, pamoja na makatibu wakuu na magavana 31 ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo.