Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta amerejelea usemi wake kuhusiana na jinsi serikali yake imejitolea kugeuza upya majeshi ya Ulinzi ya Kenya KDF.

Akizungumza kwenye sherehe ya mahafala ya makadeti katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Lanet mjini Nakuru, siku ya Alhamisi, Rais Kenyatta alisema serikali yake itazidi kutoa rasilmali za kuwezesha wanajeshi kutekeleza wajibu wao kwa njia inayostahili.

Amewataka waliofuzu kutilia maanani waliojifunza katika kipindi hicho cha miezi 36 huku akiongeza kuwa kwa kuwajumuisha maafisa kutoka Rwanda, Tanzania, Uganda na Burundi, utangamano wa kikanda unaimarishwa na kutokana na hilo, maafisa hao wanafaa kujitolea kufanya kazi yao kadri ya uwezo wao.

“Kundi hili la mwaka huu la mahafala si la Kenya pekee. Limeungana na wenzetu kutoka Tanzania, Rwanda, Uganda na Burundi. Kwa kweli, ni furaha kuwaona hapa. Bila shaka, uwepo wao hapa umeimarisha uhusiana ulio imara baina ya mataifa yetu. Natumai mtarejea nyumbani ambapo mtatumia mafunzo mliyoyapata hapa,” alisema Kenyatta.

Rais Kenyatta alisema kuwa utendakazi na uadilifu unaojitokeza kwa maafisa hao wa majeshi ya ulinzi ya KDF umepelekea majeshi hayo kukumbatiwa na Wakenya na kutokana na hilo, mahafala hao wanafaa kujibidiisha kuhakikisha kuwa hilo linasalia katika siku za usoni.

Rais Kenyatta pia amewakumbusha mahafala hao kwamba wana wajibu wa kudumisha kanuni za kazi yao ili waweze kuendeleza jina zuri la majeshi hayo ambalo limesifika kote.

Pamoja na hayo, ametaka waliohitimu wajitolee kikamilifu kutumikia taifa hili na pia kutojihusisha na mienendo isiyofaa.

Rais Kenyatta alikuwa ameambatana na Waziri wa usalama Raychelle Omamo, Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery, viongozi wakuu wa kijeshi Pamoja na viongozi wengine.