Mwakilishi mteule wa wadi kaunti ya Nyamira Fred Menge amempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kupunguza gharama ya kuunganisha nguvu za umeme kwa wakaazi hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika mji wa Nyamira, mwakilishi huyo alisema kuwa jambo ambalo Rais Kenyatta alifanya la kupunguza gharama ya kuunganisha stima ni njia mojawapo ya kuwajali wakenya.
“Namshukuru rais wetu kwa kujali maisha ya mwananchi wa kawaida na aendelee kufanya hivyo. Wananchi walikuwa wanasumbuka sana kutafuta pesa za kuunganisha stima ambazo zilikuwa mzigo kwao,” alisema Menge.
Kwa upande mwingine wakaazi wa kaunti ya Nyamira nao hawakuachwa nyuma kwa kumunga mkono mwakilishi kumshukuru rais Uhuru Kenyatta kwa kile alifanya kwa kupunguza gharama hiyo ya stima.
“Tulikuwa tunasumbuka sana kutafuta pesa hizo ambazo zilikuwa nyingi. Jambo la kufurahisha mno ni kupewa fursa ya kulipa pesa hizo kidogo kidogo. Tunasema asante kwa rais,” alisema Victor Ogeto, mkaazi wa Nyamira.
Wakaazi wa kenya wamepunguziwa mzigo wa kuunganishiwa stima kwa shilling elfu 15.
Hapo mbeleni walihitajika kulipa shillingi elfu 35 pesa ambazo zilikuwa nyingi kwa mwananchi wa kawaida
“Mimi niko na elfu kumi naenda nikope elfu tano kesho niende kwa kampuni ya Kenya Power nilipe niletewe stima kwangu kabla hawajapandisha tena,” alisema Haron Mose, mkaazi wa Nyamira.