Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kidini wameshauriwa kushirikiana kikamilifu na serikali katika hatua ya kuhakikisha kuwa matapeli wanaowatapeli waumini kanisani wanazimwa kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza jijini Kisumu alipofika katika makao makuu ya kanisa la Kiadventisti SDA kufungua rasmi jengo jipya la kanisa hilo eneo la Kanyakwar Kisumu, kiongozi wa taifa amesema serikali haina nia ya kukandamiza dini nchini na ndio sababu akaamua kuchukua hatua ya kumuagiza mwanasheria mkuu Githu Muigai kusitisha utekelezwaji wa sheria za kudhibiti makanisa nchini.

Uhuru amesema hatua ya kusitisha utekelezaji wa sheria za kudhibiti kanisa ni kutaka viongozi wa kidini husika kudhibiti shughuli zao wenyewe na kuonyesha kuwa serikali inaheshimu uhuru wa kuabudu ulivyoratibiwa kwenye katiba ya nchi.

''Kanisa liendelee kushirikiana na wadau kuleta pamoja jamii za humu nchini kutambulisha kila mmoja wetu kuwa sisi sote ni watoto wa Mungu na uzao wa taifa moja Kenya,'' alisema Rais.

Katika safari yake Kisumu miongoni mwa waliokuwa kwenye ujumbe wa Rais ni pamoja na waziri wa elimu Fred Matiang’i ambaye alimpongeza kwa kuunga mkono msimamo wa kanisa nchini.