Rais Uhuru Kenyatta alikaribishwa kwa mbwembwe, shangwe, nderemo na vifijo wakati alipowasili mjini Kisumu hapo jana.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mamia ya raia walijitokeza kando kando mwa barabara na katika kitongoji duni cha Nyalenda kwa uzinduzi wa mradi wa huduma kwa vijana wa NYS.

Raia hao, wakiwa wamepanda kwa magari na wengine kwenye miti, walifuatilia kwa makini hotuba ya rais huko Nyalenda.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook, Rais Kenyatta amesema kwamba mradi huo wa kusafisha mtaa huo utaajiri takriban vijana elfu nne.

Rais aliongezea kuwa mradi huo utajumuisha kujenga hospitali, vyoo na vituo vya polisi.

Pia aliongeza kwamba serikali yake itafanya kazi na serikali za kaunti, ili kuhakikisha matunda ya ugatuzi yanapatikana.

Akiongea katika eneo hilo ambalo linaaminika kuwa ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga, Kenyatta alisema kuwa atahudumia wakenya wote pasi na kujali ni nani ambaye alimpigia kura au la.

Kenyatta alikua kwa ziara rasmi katika kaunti ya Kisumu, ambako alifungua kongamano la pili la magavana kuhusu ugatuzi.