Rais Uhuru Kenyatta katika hafla ya awali. Picha. ctvnews.ca
Rais Uhuru Kenyatta hatimaye ameeleza sababu za kumzuia Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Feri ya Mtongwe.Katika mahojiano na runinga ya Citizen siku ya Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta alirejelea kauli yake ya awali kuwa hatakubali yeyote kumkosea heshima wakati wa hafla za rais.“Mimi sina shida na mtu yeyote lakini kamwe siwezi kubali mtu kunidharua. Ukidhani utakuja kujibizana na Rais basi wapaswa kutambua kuwa hutakubaliwa kuhudhuria hafla yangu,’’ alisema Rais Kenyatta.Kiongozi wa taifa vilevile alitetea rekodi ya Jubilee katika Mkoa wa Pwani na kupinga madai kuwa serikali yake inaendeleza miradi iliyoanzishwa na watangulizi wake, pamoja na ile iliyofadhiliwa na sekta za kibinafsi.“Mradi wa reli ya kisasa umeanzishwa na serikali, upanuzi wa barabara ya Dongo kundu unatekelezwa na serikali yangu, ukarabati katika Bandari ya Mombasa unafanywa na serikali ya Jubilee,’’ alisema Rais.Rais Kenyatta aidha alikanusha madai kuwa ana hasira na mwenye matamshi makali baada ya kunukuliwa akiwakemea Magavana Hassan Joho wa Mombasa na Josephat Nanok wa Turkana.