Rais Uhuru Kenyatta ameelezea kusikitishwa kwake na kifo cha aliyekuwa mama wa Taifa Lucy Kibaki ambaye alifariki Jumanne 26 asubuhi wakati alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali moja mjini London, Uingereza.

Share news tips with us here at Hivisasa

Lucy alikuwa mgonjwa kuanzia mwezi uliopita na alitibiwa katika hospitali za humu nchini na baadae akapelekwa London kwa matibabu zaidi.

Akitumia mtandao wa kijamii wa twitter, Rais alimtaja Lucy kuwa shujaa ambaye alijitolea kutumikia wananchi bila upendeleo.

Aliongeza kuwa mwendazake alijihusisha sana na maswala ya afya humu nchini na akachangia kwenye vita dhidi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Uhuru aliendelea kusema kuwa yeye na wakenya kwa ujumla wanaungana na jamii ya Rais mustaafu Mwai Kibaki katika wakati huu mgumukatika kuwatakia kila la heri.

"Kwa niaba ya serikali na wananchi wote, napenda kupitisha faraja zangu kwa jamii ya rais mustaafu Kibaki kwa kumpoteza mpendwa wao ambaye alikua nguzo muhimu kwa taifa,” alisema Kenyatta.

Lucy Kibaki amefariki akiwa na umri wa miaka 76, na hadi kifo chake alikuwa na watoto wanne.

Alikuwa kiongozi wa chama cha wanawake maskauti nchini na pia mwenyekiti wa muungano wa wake wa marais Afrika uliokuwa ukishughulikia juhudi za kuukabili ugonjwa wa Ukimwi.