Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzuru Kaunti ya Mombasa siku ya Jumamosi kwa ufunguzi rasmi wa Soko la Kongowea, ambalo limekua likifanyiwa ukarabati.
Soko hilo ambalo lilikua katika hali mbaya lilipata afueni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza likarabatiwe wakati alipokuwa katika ziara yake ya kaunti hiyo mapema mwakani.
Jengo jipya lililojengwa katika soko hilo linakadiriwa kuweza kuwasitiri wafanyabiashara 11,000, huku ikesemekana kuwa wachuuzi ambao hufanya kazi katikati mwa mji watapewa nafasi katika soko hilo.
Mradi huo ambao umegharamiwa na serikali ya kitaifa ulileta mvutano kati ya serikali hiyo kuu na ile ya kaunti baada ya kusemekana kuwa kaunti pia ilichangia katika mradi huo.
Hapo awali kulishuhudiwa mvutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na magavana wa pwani akiwemo Hassan Joho na Amason Kingi kuhusiana na mradi wa mwangaza mtaani ambao magavana hao walikua wameupinga.