Share news tips with us here at Hivisasa

Shughuli za kawaida zilitatizika kwa muda eneo la Kondele na mtaa wa mabanda wa Obunga jijini Kisumu siku ya Jumapili pale vijana waliziba barabara wakimtaka kiongozi wa taifa Rais Uhuru Kenyatta kuwahutubia alipokuwa akielekea kwenye makao makuu ya kanisa la SDA Kisumu.

Vijana hao ambao walikuwa na furaha walimtaka kiongozi wa taifa kuwahutubia kuhusiana na kusitishwa kwa mradi wa kazi kwa vijana na kumtaka pia awahakikishie kuwa serikali kuu inakarabati baadhi ya barabara mbovu katika eneo hilo.

Akihutubu Rais Uhuru amesisitiza kuwa watakaopatikana na hatia kuhusu matumizi mabaya ya pesa za NYS watakabiliwa kwa mujibu wa sheria.

''Tutahakikisha kuwa tumekabiliana na wale wote ambao walihusika katika wizi wa pesa na tunataka kuhakikisha kuwa pesa za kazi kwa vijana sasa zinaingia kwa vijana," Rais alisema.

''Nawahakikishia kuwa tayari mipango imeanza kuwekwa kuona vile kiwanda cha Kicomi kitafunguliwa ili kusaidia vijana kujimudu kiuchumi, kuhusu siasa hakuna haja ya sisi kama viongozi kuzozana kila mara maana tofauti ya siasa sio kuzozana wala uadui kwani wananchi wanachotegemea kutoka kwetu ni tuwafanyie kazi kuwaimarishia maisha yao,'' alisema Rais Kuhusu siasa na kufufuliwa kwa viwanda jijini Kisumu.