Magavana wa kaunti mbalimbali wakihutubia wanahabari awali [Picha/kwa hisani]
Rais Uhuru Kenyatta amewaonya magavana dhidi ya ufujaji wa fedha za umma akisema kwamba mkono wa sheria hautamsaza yeyote atakayepatikana.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika ufunguzi wa kongamano la mafunzo ya magavana huko Diani kaunti ya Kwale, alisema kwamba lazima magavana wajizatiti kulinda fedha za umma kama ilivyo kikatiba.
“Kuweni mstari wa mbele katika kulinda pesa za umma, musiwe wafujaji wa pesa hizo”,alisema Uhuru.
Aliwaonya magavana hao dhidi ya kuendeleza ufisadi ambao utalifilisisha taifa kwa ujumla.
“Acheni ufisadi ndio taifa lisonge mbele,” alisema Uhuru.
Aliongeza kuwa ili taifa kusonga mbele kimandeleo lazima kila mkenya na kiongozi kukemea ufisadi na ufujaji wa mali ya umma.
“Tutasonga mbele kimaendeleo iwapo tutakuwa mstari wa mbele kukemea ufujaji wa pesa za umma katika kila kaunti”, aliongeza rais.
Aidha, aliwasisitizia kutekeleza majukumu yao kisheria ili kulinda ugatuzi katika serikali za kaunti zilizokumbwa na changamoto ya utekelezaji katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la magavana, aliye pia Gavana wa kaunti ya Turkana, Josphat Nanok, amesisitiza ushirikiano kati ya serikali za kaunti na ya kitaifa kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.