Ripoti ya utafiti iliyofanywa na Chuo kikuu cha Pwani kuhusu gharama ya maisha imebaini kuwa asilimia 60 ya wakaazi wanaishi katika hali ya umaskini licha ya kujimudu na kupata shilingi 100 kwa siku.
Ripoti hiyo imebaini kuwa idadi kubwa ya familia za kurandaranda mijini hutumia fedha hizo kidogo kwa ununuzi wa dawa za kulevya na kuchangia kuwepo kwa ukosefu wa usalama.
Akizungumza katika hafla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumanne, mkurugenzi mkuu wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu Huria, Yusuf Lule, alisema kuwa baada ya kupitia ripoti hiyo, amebaini kuwa asilimia 60 ya famila zinaoishi mtaani ni wanaume huku wengine ikiwa ni wanawake na watoto.
Lule alisema kuwa sababu kuu za familia hizo kuishi barabarani na katikati ya mji ni kutokana na umaskini, ukosefu wa ajira, ukosefu wa mazingira safi na kulelewa na mama wa kambo.
Mwanahakati huyo alisema kuwa amehuzunishwa mno na ripoti hiyo na kuahidi kuandaa mikakati mwafaka ya kuhakikisha kuwa idara husika inaingilia kati swala hilo na kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kubadili maisha ya Wakenya wanaohangaika.
"Kama shirika la kijamii sisi tumehuzunishwa na ripoti hii kuwa wengi wa wakaazi wanaishi katika hali ngumu ya maisha na kurandaranda mtaani kutokana na ukosefu wa ajira na mazingira duni. Hali hii inastahili kusitishwa,” alisema Lule.