Jaji mkuu David Maraga./NMG

Share news tips with us here at Hivisasa

Jaji mkuu David Maraga amewataka wakenya wenye ushahidi wa madai ya rushwa dhidi ya maafisa wa Mahakama kupiga ripoti katika tume ya huduma za mahakama nchini JSC.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Maraga alisema kuwa kuna maafisa wa mahakama ambao wanakosa maadili mema lakini akawataka wakenya wenye ushahidi kujitokeza na kupiga ripoti. 

“Wakati mwingine tuna maswala ya kukosa maadili mema lakini si wote wafisadi ndiposa tunahitaji msaada wenu,’’ alisema Maraga.

Maraga aliwaonya wafanyikazi wa mahakama dhidi ya kujihusisha ya visa vya ufisadi na kusema kuwa tume ya huduma za mahakama nchini itamchukulia hatua yeyote atakayepatikana na makosa.

Maraga alikuwa akizungumza na wahudumu wa mahakama, chama cha wanasheria nchini na maafisa wa huduma za mahakama baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mnara wa mahakama mjini Mombasa utakaogharimu shilingi milioni 445.

Maraga pia aliishukuru serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kupeana ardhi kwa kaunti ndogo zote sita kwa ujenzi wa mahakama ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za mahakama kwa gharama ya chini. 

Maraga alimaliza ziara yake ya siku tatu pwani ya Kenya ambapo alianzia kaunti ya Kwale siku ya Jumatatu.