Naibu gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Ruto ametoa wito kwa kila mmoja kulikumba taifa hili na hasa vikosi vya usalama katika maombi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika hafla moja mjini Nakuru Jumanne, Ruto amesema kuwa wakati huu ambapo taifa linaomboleza kwa kupoteza wanajeshi katika shambulizi ni vyema kujikita katika maombi.

"Tunasema pole sana na tunazidi kurai kila mmoja tusimame na famili zao katika maombi," alisema Ruto.

Na huku uchaguzi mkuu wa 2017 ukikaribia, naibu gavana huyo wa Nakuru ametoa wito kwa kila mmoja katika jamii kujisajili kama wapiga kura ili kutoa nafasi ya uongozi bora.

"Huwezi chagua kiongozi kama hauna kitambulisho cha kitaifa na pia kura kwa hivyo nawarai tafadhali mjiandikishe ndiposa mshiriki maamuzi muhimu katika taifa hili," alisema Ruto.

Alisema kuwa ana imani atarejea afisini pamoja na gavana Kinuthia Mbugua ili kukamilisha miradi walioanzisha ya maendeleo katika kaunti ya Nakuru.

Wakati uo huo Ruto amedokeza kwamba atawania ugavana katika uchaguzi mkuu wa 2022, suala ambalo linaonekana changamoto kwa mbunge wa Nakuru mjini David Gikaria ambaye pia amekiri kuwania kiti hicho 2022.

"Naambia Gikaria kwamba ajipange kwani 2022 pia nami nimo kwenye kinyang'anyiro cha ugavana kwa hivyo tutakutana huko na si mbali hata nimetosha," alisema Ruto.

Wakati uo huo ametoa wito kwa kila mmoja katika kaunti ya Nakuru kutia bidi hasa mwaka huu kwa mustakbali wa kaunti na taifa kwa jumla.