Naibu Rais William Ruto ameishutumu afisi ya mwendesha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Ruto anataka afisi hiyo kuchunguzwa kwa madai ya kuhujumu utoaji wa haki kama vile kudai uroda wakati wa kufanywa kwa uchunguzi wa kesi yake.
Upande wa utetezi wa Ruto ulidai kuwa timu ya Bensouda ilidai ngono ili kupata ushahidi wa uongo.
Madai hayo yalijitokeza siku ya Jumatatu wakati upande huo wa utetezi chini ya uongozi wa mwanasheria Karim Khan, uliwasilisha ombi katika Mahakama ya ICC wakitaka uchunguzi kufanywa dhidi ya utendakazi wa afisi ya mwendesha mashtaka wakati wa kesi ya Naibu Rais William Ruto.
Ruto alikuwa ameshtakiwa kwa madai ya kuhusika katika visa vya jinai ambavyo vilitokana na machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Ruto alikuwa miongoni mwa Wakenya wengine watano waliokuwa wameshtakiwa katika mahakama hiyo yenye makao yake huko Hague, Uholanzi.
Kesi dhidi ya Wakenya hao wasita zilitupiliwa mbali.
Ruto alijitosa kwenye ulingo wa siasa katika Kaunti ya Uasin Gishu alipohudumu kwa mara ya kwanza kama Mbunge wa Eldoret Kaskazini kati ya 1997-2013.
Ruto ametajwa na wengi kama kiongozi wa jamii ya Kalenjin.