Serikali ya kaunti ya Nakuru imewahimiza wakaazi kujitokeza kwa wingi wakati wa kushirikishwa kwao katika mpango wa kuandaa bajeti ya mwaka huu wa kifedha 2016-2017.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika mahojiano na redio moja ya humu nchini siku ya Jumanne usiku, naibu gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Ruto, alisema mwezi Mei watazunguka katika kila wadi za kaunti ya Nakuru kuyasikiliza na kuyanakili matakwa ya wananchi ili kuyajumuisha katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha.

“Tulipoingia mamlakani tulikuwa na awamu ya kwanza na tulitengea kila wadi shilingi milioni 12, awamu ya pili shilingi milioni 25 na sasa kila wadi itapata shilingi milioni 12 ya maendeleo,” Ruto alisema.

Alisema kila mwakilishi wa wadi anatarajiwa kuwasilisha miradi mbalimbali katika hazina ya kaunti ambayo wananchi wamekuwa wakitaka kuanzishiwa au kukarabatiwa na pia katika ziara zao katika kila wadi, watazipitia tena matakwa hayo ili kuhakikisha hakuna ubadhirifu wowote unashuhudiwa katika mwaka huu wa kifedha.

Ruto alisema baada ya kuwasilishwa kwa matakwa hayo, watayatadhmini kisha kuzitekeleza punde tu baada ya kukamilika kusomwa kwa bajeti.