Viongozi wa chama cha KANU kutoka kaskazini mwa Bonde la Ufa sasa wanamtaka naibu wa raisi William Ruto kuomba msamaha kwa madai aliyotoa dhidi ya mwenyekiti wa chama hicho, Gideon Moi.
Viongozi hao, wakiongea mjini Eldoret, wameinga madai kwamba Moi anamwombea naibu wa raisi afungwe kwenye mahakama ya uhalifu ya kimataifa ya ICC, ili awe na usemi wa kisiasa katika eneo la bonde la ufa.
Wakiongozwa na mshirikishi wa chama hicho katika eneo Jonathan Bii, walisema kwamba mambo kama hayo kamwe hayakubaliki.
Pia viongozi hao wamesema kuwa matamshi hayo siyo tu kinyume na tamaduni na mila ya jamii ya Kalenjin, bali pia yanalenga kuigawanya jamii hiyo ambayo wamesema kwamba imekua ikimuunga mkono Ruto.
Viongozi hao walisema kuwa iwapo Ruto alikuwa na ripoti kama hiyo, angetumia mbinu nyingine kuiwasilisha na wala sio kupitia kwa vyombo vya habari.
Kuhusu siasa za 2017, Bii amesema kwamba Moi ana haki ya kuwania kiti chochote cha kisiasa, kikiwemo kile cha uraisi, kama mkenya mwingine yeyote.
Joto la ubabe wa kisiasa limepamba moto katika eneo la bonde la ufa, huku ripoti zikionyesha kwamba hivi majuzi, Moi na gavana wa kaunti ya Bomet Isaac Ruto walikutana kupanga mikakati ya kisiasa katika kinyang'anyiro cha mwaka wa 2017.