Mwenyekiti wa chama cha Jubilee Kaunti ya Mombasa Ali Mwatsahu akiwahutubia wanahabari katika hafla ya awali. Picha/ kenyanewsagency.go.ke
Wanachama wa Jubilee wamemtaka Naibu wa Rais Wiliam Ruto kuingilia kati mzozo wa uongozi unaoshuhudiwa baina ya viongozi wa chama hicho katika Kaunti ya Mombasa.Wakiongozwa na mwenyekiti Ali Mwatsahu wafuasi hao walilalamika kuwa hakuna ushirikiano bora baina ya wanachama hao tangu kupatanishwa kwa mgombea wa kiti cha ugavana Suleiman Shahbal na mgombea mwenza Anania Mwaboza.Mwatsahu alisema kuwa kuna haja ya Ruto kulishugulikia swala hilo mara moja.Aidha, Mwatsahu ameelezea wasiwasi wake kwamba endapo swala hilo halitatatuliwa mapema, basi huenda kukashuhudiwa mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho na hata kuzua taharuki miongoni mwa wafuasi.“Hatua ya haraka isipochukuliwa tutakuwa tumepoteza mwelekeo wa kisiasa hususan kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi mkuu, hatua itakayotusababisha kukosa umaarufu na hata nyadhifa mbalimbali za uongozi ifikapo mwezi Agosti,” alisema Mwatsahu.Wanachama hao walisema ushirikiano bora ndio utakao saidia kuibandua mamlakani serikali ya Gavana Hassan Joho.