Naibu Rais William Ruto amewaonya maafisa wa polisi wanaoshirikiana na walanguzi wa mihadarati kuwa watakabiliwa kisheria.
Akiwahutubia wanahabari jijini Mombasa siku ya Jumanne, Ruto alisema kuwa serikali ya Jubilee itafanya kila iwezalo kukabiliana na janga la ulanguzi na utumizi wa dawa za kulevya.
“Tutawakabili maafisa wa polisi wanaohusika katika biashara hii haramu pamoja na walanguzi wenyewe mpaka tupate suluhu la tatizo hili,” alisema Ruto.
Aidha, alisema kuwa tayari wanataarifa za kijasusi kuhusu maafisa hao, na kuongeza kuwa watakabiliwa na mkono wa sheria hivi karibuni.
Ruto alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa vijana wanajinasua katika jinamizi hilo la utumizi wa mihadarati.
Vile vile, alisema kuwa vita hivyo pia vinalenga kukabiliana na tatizo la ugaidi, kwa vile fedha zinatopatikana kupitia biashara ya mihadarati hutumiwa kufadhili makundi ya kigaidi nchini.
Ruto alisema serikali itashirikiana na mataifa ya nje katika vita hivyo, ili kuhakikisha walanguzi hao wanachukuliwa hatua za kisheria.
Wakati huo huo, amepinga madai kuwa vita dhidi ya utumizi wa mihadarati vinatumika kisiasa ili Jubilee kujipigia debe Pwani.