Naibu Rais William Ruto akiwahutubia wakaazi wa Kilifi siku ya Alhamisi. [Picha/ PSCU]
Naibu Rais William Ruto ameukosoa mrengo wa NASA kwa kueneza propaganda kuhusu serikali ya Jubilee.
Ruto amesema kuwa Nasa haina malengo yoyote ya manufaa kwa raia na kudai kuwa viongozi wa mrengo huo wanajali tu matumbo yao.
“Nasa hawana nia ya kuendeleza maisha ya mwananchi bali lengo lao kuu ni kujinufaisha kibinafsi,” alisema Ruto.
Akizungumza huko Lunga Lunga Kaunti ya Kwale, Ruto aliikashifu Nasa kwa kueneza propaganda zisizokuwa na msingi kwa nia kuharibia jina serikali ya Jubilee.
“Hawana la maana wanaongea wakiwa jukwaani ila kulaumu serikali kila uchao,” alisema Ruto.
Ruto amewataka wanachi kutosikiza kasheshe za Nasa kamwe na badala yake kuunga mkono Jubilee kwenye uchaguzi ujao.
“Pigieni kura serikali ya Jubilee iweze kupita tena na kuwaongoza kwa awamu ya pili. Musisikize wale jamaa wa Nasa,” alisema Ruto.
Haya yanajiri huku viongozi wakuu wa kaunti hiyo wakiongozwa na Gavana Salim Mvurya, naibu wake Fatuma Achani, mwakilishi wa wanawake Zainab Chidzuga wakiendelea kupigia debe serikali ya Jubilee iweze kuongoza kwa awamu ya pili.