Naibu wa Rais William Ruto amekata kimya chake kuhusiana na kifo cha mwanabiashara wa Nairobi Jacob Juma.
Ruto aliyekuwa katika mahojiano ya kipekee katika runinga ya Citizen hapo Jumanne usiku alikariri kuwa yeye ni mweupe kama pamba katika patashika lote linalohusiana na kifo cha mwanabiashara huyo.
"Naam, nafikiri tulimpoteza Jacob Juma. Na nataka kuwaambia wakenya na taifa lote kwa jumla kuwa sihusiki kivyovyote vile na maisha wala kifo cha Juma," alisema Ruto.
"Nina hakika kama jinsi jua huchomoza kila siku basi pia walio muua Juma watapatikana na kushtakiwa," aliongeza Ruto.
Aidha Ruto pia alisisitiza kuwa wanasiasa wa magharibi ya Kenya wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo, ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kumuhusisha na kifo ya mwanabiashara huyo wanastahili waje katika mahojiano ya runinga ili waeleze kinaganaga kwanini wanamuhusisha na kifo hicho.
"Nadhani itakuwa jambo la busara iwapo tutatenga mda katika kituo hichi ili Jirongo naye aje hapa aelezee taifa ni nini anamaanisha kwa kunuhusisha na sakata ya kifo cha Juma," Ruto alisema.
Fauka ya hayo Ruto alikiri kuwa yupo tayari kuhojiwa na maafisa wa usalama iwapo watahitaji mchango wake katika kukitegua kitendawili cha kifo hicho.
"Iwapo polisi watahitaji usemi wangu kuhusiana na kifo cha Jacob Juma niko tayari wakati wowote kushirikiana nao, kwasababu mimi ni mwanainchi anyaeithamini sheria na pia nataka swala hili lipate suluhu ya kudumu," alisema Ruto.
Naibu Rais pia alilama akisema kuwa wanasiasa wa mrengo wa upinzani wamekuwa wakimtumia yeye kama nguzo ya kuwakilisha kutojiweza kwao huku wakimtaja kama kizingiti katika maendeleo ya kitaifa.
"Nimekuwa kama kisababu cha masaibu ya mrengo wa upinzani, na wao hutafuta kila jambo kunihusisha na masaibu yao," alisema Ruto.