Naibu wa Rais William Ruto katika hafla ya awali. [Picha/ PSCU]
Naibu Rais William Ruto amesema kuwa viongozi wa upinzani ndio waliohusika katika unyakuzi wa ardhi eneo la Pwani hasa walipokuwa katika serikali zilizopita.
Ruto alisema kuwa viongozi hao kwa sasa wanajidai kupinga unyakuzi wa ardhi, ilihali wao ndio waliojihusisha na wizi wa mashamba ya Wapwani.“Wao ndio walinyakuwa mashamba mengi ya Wapwani lakini sasa wamegeuka na kuanza kuilaumu Jubilee,” alisema Ruto.Akizungumza mjini Lamu siku ya Jumatano, Ruto aliwataka viongozi hao kukoma kulaumu Jubilee ilhali inajizatiti kutatua swala la unyakuzi wa ardhi nchini.“Jubilee tunajitahidi kumaliza unyakuzi wa ardhi lakini wapinzani wetu bado wanatukosoa pasi kufikiria,” alisema Ruto.Kwa upande wake, Rais Uhuru Kenyatta alisema serikali yake itawapa wakaazi wa Lamu hatimiliki zaidi ya 11,000 hivi karibuni, kama njia mojawapo ya kumaliza utata wa ardhi katika kaunti hiyo.Akizungumuza katika mkutano wa kisiasa katika eneo la Mkunguni mjini Lamu, Rais Uhuru alisema swala tata la ardhi litatuliwa punde wakaazi watakapopata hati miliki.