Naibu Rais William Ruto amewaahidi Wakenya kuwa uchaguzi wa 2017 utakuwa wa huru, haki na amani, huku akiwahimiza kutowapa sikio viongozi wanaoeneza matamshi ya chuki na ukabila.
Kwa wiki moja sasa wanasiasa wa mrengo wa Jubilee na Cord wamekuwa wakitupiana cheche za maneno kuhusu mpango wa kuiba kura katika uchaguzi ujao.
Joto hilo linaaminika kuibuliwa na matamshi ya mwanasiasa kutoka Mombasa, Shahbal Suleiman, aliyenukuliwa akisema kuwa Jubilee itashinda uchaguzi huo kwa kutumia njia yoyote ile, matamshi aliyoyatoea mbele ya Naibu Rais William Ruto mjini Kilifi wikendi iliyopita.
Hata hivyo, Ruto sasa amevunja ukimya na kusema kuwa yeyote anayetoa matamshi kama hayo anafaa kukamatwa na kushtakiwa bila kujali mrengo anaougemea.
“Wakenya wanataka amani kwa hivyo yeyote anayelenga kuvuruga amani hiyo kwa maneno yasiyofaa atakumbana na mkono wa sheria,” alisema Ruto, akizungumza nyumbani kwake Sugoi kaunti ya Uasin Gishu siku ya Alhamisi, alipotembelewa na wanasiasa kutoka Nyamira na Kisii.
Ruto aliwataja wanaodai kuwa Jubilee inapanga kuiba kura kuwa watu wanaogopa ushindani.
“Uchaguzi utakuwa wa huru, haki na amani. Hicho ndicho kitu ambacho Mkenya mpiga kura anahitaji kisheria,'' aliongeza Ruto.
Naibu Rais aliwahimiza Wakenya kukumbatia umoja, undugu na upendo wala wasikubali kugawanywa kwa msingi ya kisiasa na kikabili.
Siku ya Jumatano, kinara wa Cord Raila Odinga alidai kuwa serikali inapanga kutumia pesa na madaraka kushinda katika uchaguzi ujao, madai yaliyopingwa vikali na mrengo wa Jubilee ukiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Adel Duale.