Serikali kuu itaikarabati barabara ya Kibunja hadi Kiptagich ili kurahisisha usafiri kwenye barabara hiyo ambayo imekuwa kero kubwa kwa wenyeji wa maeneo bunge ya Molo, Kuresoi Kusini na Kuresoi Kaskazini.
Naibu gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Rutto amesema serikali kuu imeratibu ukarabati wa barabara hiyo kuanzia mwezi Machi, 2016, huku wanakadarasi wakitarajiwa kuanza kazi hiyo mara moja.
Ruto akiongea na wakaazi katika eneo la Olenguruone amesema serikali ya jimbo la Nakuru imekuwa ikitoa kima cha shilingi milioni 25 kila mwaka wa kifedha kwa kila wadi ili kufadhili miradi ya maendeleo.
Watu wanauliza kwa nini hatukarabati barabara hii. Ukweli ni kwamba barabara hii iko chini ya serikali kuu, lakini kandarasi tayari imetolewa na serikali kuu itaikarabati mwezi Machi,” alisema bw Ruto.
Naibu huyo wa gavana amewataka wananchi katika kila eneo la uwakilishi kufuatilia jinsi fedha hizo zinavyotumika ili maeneo yao yaweze kufaidika na miradi watakayopendekeza.
“Sisi kama kaunti tunatoa shilingi milioni 25 za kila wadi kwa maendeleo, kwa hivyo uache kulalamika ukiona wadi nyingine imeendelea, nyinyi na MCA wenu ndio muamue jinsi ya kutumia fedha hizo,” alisema.
Amesema kila wadi katika kaunti ya Nakuru hupokea shilingi milioni 2 za basari ili kuwapiga jeki wanafunzi ambao hulemewa na masomo kwa sababu ya ukosefu wa karo.