Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwa muda mrefu kumekuwa na utani hasa kutoka kwa watu wa bara na maeneo mengine ya taifa kwamba watu wa Mombasa ni wavivu wasiopenda kufanya kazi.

Hilo siwezi kudhibitisha, lakini ukweli ni kwamba tabia nyingi zinazochangia mfumo wa maisha unaoonekana miongoni mwa wakaazi wa mji wa Mombasa zinatokana na tamaduni za mji huu, ambazo zimekuwepo tokea zamani.

Je ushawahi kujua kwamba zamani wanawake mjini Mombasa hawakuruhusiwa kufanya kazi wala biashara yoyote nje ya boma.

Nilikutana na msomi wa historia ambaye pia ni mzaliwa na mkaazi wa Mombasa Dkt Allawy Abzein, aliyenieleza kwamba utamaduni huo uliwafanya wanawake wengi kuishi na dhana kwamba mwanamke hawafai kufanya kazi.

“Wanaume hasa waliokuwa na mali walikuwa hawaruhusu wake zao kutoka nje kufanya biashara, na hiyo ilifanya wanawake wengi kujua kwamba jukumu la kuchuma sio lao bali ni la wanaume pekee,” alisema Dkt Allawy.

Msomi huyo alieleza kwamba hali hiyo imewafanya wanawake wengi mjini Mombasa na Pwani kwa ujumla kubaki nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na wenzao wa kutoka bara.

Alisema kuwa ilikuwa ni makosa makubwa mwanamke kuonekana barabarani akizungusha bidhaa au kutumia muda mwingi akiwa nje ya boma.

Hata hivyo, alisema kwamba baada ya maisha kubadilika na elimu ya kisasa kuanza kukita mizizi katika jamii, dhana hiyo imeanza kuondoka miongoni mwa jamii za Mombasa ingawa wamejipata wamechelewa zaidi.

Bi Amira Said, mkaazi wa Old Town Mombasa, ambaye ni mmoja wa washauri wa wasichana na wanawake wa eneo hilo, alisema ukosefu wa elimu ulizidi kuwakandakamiza zaidi wanawake eneo hilo, lakini sasa baadhi yao hasa wale waliosoma wameanza kubadili mambo.

Dkt Allawy kwa upande wake alisema wakati umefika kwa wanawake Mombasa kujitokeza na kufanya biashara kwani kuna fursa nyingi zinazowapita.

Aidha, amewashauri kuwa wabunifu zaidi na kufikiria biashara kubwa kubwa badala ya kutegemea uuzaji wa vyakula vya bei rahisi kama vile kaimati, viazi karai, samaki na kadhalika.