Mbolea inayoshukiwa kuwa ya wizi inayogharimu shilingi milioni 4, 527,000 kutoka bodi ya nafaka na mazao nchini NCPB, ilinaswa usiku wa kuamkia Alhamisi kwenye ghala la mahindi la kibinafsi katika eneo la Railways Go Down mjini Nakuru.
Mbolea hiyo iliyonaswa kupitia vidokezo kutoka kwa wananchi, inadaiwa kuibwa na dereva mmoja wa trela ambaye husafirisha bidhaa kutoka mjini Nairobi kuelekea maeneo ya Magharibi, ambaye ni mmiliki wa ghala hilo kwa jina Wilkah.
Dereva huyo kwa sasa amesimamishwa kazi na alizuiliwa na polisi kufuatia tukio hilo hadi pale uchunguzi utakapomilika.
Kulingana na mwenyekiti wa NCPB Geofrey King’ang’i, mifuko hiyo 3,115 ya mbolea aina ya DAP kutoka kwa serikali ni miongoni mwa mbolea zinazouziwa wakulima kwa bei nafuu huku wahalifu wakijinufaisha kupitia kwayo.
“Tumefanikiwa kupata mifuko zaidi ya elfu tatu, yenye uzito wa kilo hamsini kila moja. Ni ufanisi mkubwa kudungua sakata kama hii, ambayo inafanya wakulima wasifaidike na pembejeo ambayo serikali inawapa kwa bei nafuu,” King’ang’i akizungumza mjini Nakuru Alhamisi alisema.