Swala la ukosefu wa stakabadhi za elimu miongoni mwa wananchi limetajwa kama kizingiti kikubwa katika maendeleo kwa wakaazi katika kaunti ya mombasa na ukanda wa Pwani kwa jumla.
Akitoa kauli hiyo mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Seneta wa kaunti hiyo Hassan Omar Sarai amesema kuwa hali hii imechangia kuzorota kwa hali ya uongozi bora kwani amedokeza kuwa kiongozi mwenye kuleta mabadiliko na manufaa kwa jamii ni lazima awe na elimu ya kutosha.
Aidha Seneta huyo amesikitishwa na hali ya jinsi watu wengi katika kanda ya Pwani hushindwa kuwania nyadhifa za uongozi kwa kutokana na viwango duni vya elimu.
Kulingana na Sarai swala la stakabadhi pia limechangia pakubwa swala la ukosefu wa ajira kwa vijana hususani katika mwambao wa Pwani.
"Tumeona maswala ya maendeleo yakirudi nyuma kutokana na kuwa idadi kubwa ya wakaazi wa Pwani hawana stakabadhi za elimu na swala hili lazima tulifikirie kwa kina ili tulete mabadiliko Pwani," alisema Sarai.
Hata hivyo ameonyesha matumaini yake kuwa chuo kikuu kinacho paniwa kujengwa katika eneo la Mackinon Road kitasaidia kuboresha viwango vya elimu katika mwambao wa Pwani.