Hakmashauri ya Bandarini nchini KPA imesema kuwa imetenga takriban shilingi milioni mia moja kufanya ukarabati wa eneo la kupokea wageni na mizigo bandarini humo.
Sehemu hiyo ya kisasa inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuwahudumia wageni wengi zaidi tofauti na sasa, na pia kurahisisha zoezi la kuwapokea wageni hao, ambao wanaoenekana kumiminika eneo hilo la Pwani kujivinjari.
Akiongea katika wakati wa kupokea meli ya kitalii ya Silver Clouds siku ya Jumanne, afisa wa mawasiliano bandarini humo Hajji Masemo alisema kuwa mpango huo unatarajiwa kuanza mwezi April mwaka huu.
“Tayari tumeshatenga pesa hizo na shughuli iko tayari. Kuanzia mwezi Machi mwaka huu tutaanza mchakato wa kutafuta wanakandarasi ili ifikiapo Aprili mradi uanze,” alisema Masemo.
Afisa huyo aliwaambia wanahabari kwamba eneo hilo litakuwa la kifahari na litatoa taswira nzuri kwa wageni waliozuru eneo hilo kupitia Bandari, na kuongeza kuwa watalii wanapovutiwa, hupata hamu ya kurudi tena kwa mara ya pili.
Masemo aidha alisema kuwa ujenzi huo utaleta ajira kwa vijana wengi wa eneo hilo ambao hawana kazi kwa sasa.
Mwakilishi wa bodi ya utalii nchini Allan Njoroge pamoja na mwenyekiti wa wadau wa utalii Pwani Mohamed Hersi pia walihudhuria hafla hiyo ya kuwapokea watalii hao kutoka kisiwani Zanzibar.
Hersi alisema kuwa meli hiyo iliyobeba takriban watalii 190 ni ya pili mwaka huu na ya nane tangu msimu wa utalii kuanza, na kutaja ziara hiyo kama hatua njema kwa sekta hiyo.