Wizara ya Utalii nchini imesema kuwa inakadiria sekta hiyo itaimarika katika kanda ya Pwani kwa asilimia 20 mwaka huu, kutokana na mikakati ambazo ziliwekwa mwaka wa 2015.
Akizungumza katika mkutano wa washikadau katika sekta ya utalii ulioandaliwa mjini Mombasa siku ya ijumaa, Waziri wa utalii nchini Najib Balala, alisema kuwa kufikia sasa tayari sekta ya utalii imeboreka ikilinganishwa na wakati kama huu mwaka uliopita.
Balala alisema kuwa zaidi ya asilimia 30 za hoteli zilizoko Mombasa, Kwale, Kilifi na Malindi zimetengwa kwa watalii.
“Sekta ya utalii itapigwa jeki kwa kuzinduliwa kwa ndege za moja kwa moja kutoka nchini Kenya hadi nchi ya Poland,” alisema Balala.
Aidha, Balala alisema kuwa ziara ya Rais wa Marekani Barrack Obama na kiongozi wa kanisa la kikatoliki Papa Francis mwaka uliopita zimechangia pakubwa katika ukuzaji wa sekta ya utalii.
kwa upande wake, mkuu wa Idara ya Utalii katika Kaunti ya Mombasa Binti Omar alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa imeweka mikakati ya kutathmini utendakazi wa hoteli zote ambazo zinakibali ya utalii ili kuboresha sekta hiyo.