Wadau katika sekta ya utalii wamesema kuwa utalii umeimarika katika eneo la Pwani kutokana na kuboreshwa kwa usalama.
Mkurugenzi wa Hoteli za Heritage Mohammed Hersi amesema kuwa hali hiyo imetokana na kushuhudiwa kwa hali ya utulivu, ambapo katika muda wa miaka miwili iliyopita, hakujashuhudiwa visa vyovyote vya mashambulizi ya kigaidi kinyume na hapo awali.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika kikao cha pamoja na kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed, Hersi alisema kwa sasa watalii wengi wanaweza kuzuru eneo la mji wa Kale ambalo lilikuwa likikumbwa na visa vya utovu wa salama, ishara tosha kwamba usalama umeimarika.
Aidha, alidokeza kuwa asilimia themanini ya watalii waliomo katika hoteli nyingi za eneo hilo ni raia wa humu nchini, wengi wao wakitoka jijini Nairobi.
“Kwa sasa tunaweza tembeza watalii katika mji wa Kale kutokana na kuboreshwa kwa usalama. Hili linawezesha wenyeji kunufaika kutokana na utalii,” alisema Hersi.
Mwenyekiti wa chama cha wadau wa hoteli kanda ya Pwani Victor Shitakha alisema kuwa mwishoni mwa mwaka huu kutakuwa na wajumbe wataolekea mjini Monaco, ambapo watashawishi wadau wengine wa kimataifa kuipa Kaunti ya Mombasa fursa ya kuwa mwenyeji wa kongamano la Skul mwaka wa 2018.
Kongamano hilo lilitarajiwa kuandaliwa humu nchini mwaka jana, lakini Kenya ikakosa nafasi hiyo kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyokuwa yakishuhudiwa mara kwa mara.
Hata hivyo, wadau hao walionyesha kughadhabishwa kwao na msongamano wa magari unaoshuhudiwa katika barabara kuu ya Mombasa-Malindi, haswa eneo la Marikani na Kibarani, wakisema hali hiyo inachelewesha safari za watalii.