Seneta wa kaunti ya Nyamira Okong'o Mong'are ameishtumu vikali idara ya ununuzi na utoaji zabuni katika kaunti ya Nyamira baada ya madai ya ufisadi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumamosi, Mong'are alishangazwa na sababu iliyosababisha serikali ya kaunti hiyo kuweka tangazo la utoaji zabuni kwenye gazeti moja la humu nchini na kisha baadaye kufutilia mbali utoaji zabuni mbalimbali.

“Kuna zabuni zilizotolewa mwaka jana na tunashangazwa ni kwa nini serikali ilifutilia mbali zabuni zinazogharimu shillingi millioni 300 ikizingatiwa kwamba tayari tangazo la utoaji zabuni hizo lilikuwa limewekwa kwenye gazeti moja la na ambalo halina usomi mkubwa," alishangazwa Mong'are.

Mong'are aidha ameitaka idara hiyo kuhakikisha kwamba tangazo la utoaji zabuni hizo linatolewa upya kwa maana idara hiyo haikufuata maagizo yanayozingatiwa wakati wa utoaji zabuni.

“Serikali haikufuatilia maagizo na sheria za utoaji huduma za zabuni, na sharti waanzishe upya shughuli hiyo na tayari wanakandarasi ambao tayari walikuwa wamelipa pesa zao wasiagizwe kulipa pesa zingine upya," aliongezea Mong'are.