Seneta wa kaunti ya Nyamira Okong'o Mong'are ameunga mkono hatua ya kesi ya jinai iliyokuwa ikimkabili naibu rais William Ruto na mtangazaji Joshua Sang kutupiliwa mbali. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye uwanja wa shule ya upili ya Nyabikomo kwenye eneo wadi ya Kiabonyoru siku ya Ijumaa wakati wa hafla ya kuchangisha pesa zakufadhili miradi ya shule, Mong'are aliwapongeza wakenya kwa maombi yao ya kuitaka mahakama hiyo kutupilia mbali kesi hiyo. 

"Kwa kweli wakenya walichukua nafasi ya kumwombea naibu rais Willam Ruto na mtangazaji Joshua Sang ili kesi zao zitupiliwe mbali kule Hague, na ni furaha yetu kwamba kesi hizo zimetupiliwa mbali kwa maana tunahitaji utangamano tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao," alisema Mong'are. 

Hata hivyo, seneta Mong'are aidha aliitaka serikali ya kitaifa kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wamefidiwa ili kurejelea maisha yao ya kawaida. 

"Ni afueni kwa serikali kwamba kesi ya Sang na Ruto imetupiliwa mbali, na ndio sababu rais Kenyatta ana mipango ya kufanya hafla ya maombi ya pamoja kwenye uwanja wa michezo wa Afraha kule Nakuru, ila kabla ya hilo analostahili kufanya ni kuhakikisha waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wamefidiwa," aliongezea Mong'are.