Seneta wa Mombasa Hassan Omar amemkosoa mshirikishi wa usalama katika Ukanda wa Pwani Nelson Marwa kwa kile alichokitaja kama utawala wa kikoloni dhidi ya viongozi wa kaunti waliochaguliwa na wananchi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta Omar alidai kuwa Marwa amekuwa akitatiza utendakazi wa viongozi wa kaunti, huku akimkosoa kwa kutumia nguvu jambo alilosema kuwa limeleta mzozo miongoni mwao.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Omar alidokeza kuwa kulingana na katiba mpya, viongozi wa kaunti akiwemo gavana na wengine wana mamlaka ya kuendesha shughuli za uongozi bila kutatizwa na afisa yeyote wa serikali.

“Siamini kwamba kulingana na katiba mpya kiongozi aliyechaguliwa na wananchi anafaa kuwa chini ya mamlaka ya mtu mwingine anayetekeleza majukumu yake kwa njia ya kikoloni,” alisema Omar.

Wakati huo huo, Omar alisema kuwa licha ya kwamba Kaunti ya Mombasa ina viongozi wa upande wa upinzani, Marwa hafai kuchukua fursa hiyo kuwanyanyasa viongozi hao.

Seneta huyo alisema kwamba wananchi wa Mombasa wanaweza kukosoa serikali ya kaunti iwapo watashuhudia hali inayowakera na wala sio jukumu la mshirikishi wa usalama kufanya hivyo.

“Hata kama hakuna upinzani, wananchi wenyewe wanaweza wakaona kile kinachoendelea kwa hivyo kama kuna makosa wenyewe watakosoa,” aliongeza Omar.

Kauli ya Seneta Omar inajiri huku mzozo ukiendelea baina ya mshirikishi wa uslama katika Ukanda wa Pwani Nelson Marwa na viongozi wa Pwani akiwemo Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi.