Kufuatia visa vya mauaji ya kinyama kuendelea kuripotiwa katika maeneo mengi kaunti ya Nyamira, sasa Seneta wa kaunti hiyo, Okong'o Mong'are, amejitokeza kuishtumu wizara ya usalama wa ndani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwahutubia wakazi wa Nyabara Ibere katika wadi ya Bonyamatuta, kaunti ya Nyamira siku ya Jumamosi, Mong'are alimwomba waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery kuwahakikishia wakazi wa Nyamira usalama wao.

 "Nataka kuiambia serikali kuu kama hawatoweza kuweka usalama wa kutosha kwa watu wetu, wacha watuambie wameshindwa kuweka usalama ili tujue la kufanya maana watu wetu hawawezi kuuliwa kiholela," alisema Mong'are. 

Seneta huyo aidha alimpa Nkaissery ilani ya mwezi mmoja ili kuwaondoa kamanda wa oparesheni za polisi Kalimbo Mwandoye na kamishna wa kaunti hiyo Josephine Onunga iwapo hawataimarisha usalama. 

"Nimempa waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery makataa ya mwezi mmoja kuwahamisha kamanda wa oparesheni za polisi Kalimbo Mwandoye na Kamishna Onunga iwapo watashindwa kutuhakikishia usalama kwa maana jukumu la usalama kwa wananchi ni la serikali kuu," aliongezea Mong'are.