Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o ameiomba serikali ya kitaifa kuchukua wadhifa wa usimamizi wa chama cha KTDA kutokana na suala la wakulima kutolipwa pesa za bakshishi kwa kiwango kinachostahili kwa mda mrefu.
Akiongea na wanahabari katika mji wa Nyamira siku ya Ijumaa, Okong’o alisema aliunga mkono kampuni moja iliyokuwa ikichunguza chama hicho cha KTDA, kufuatia madai ya ujanja na kukiri kuwa chama hicho huaribu bei ya majani chai inapouzwa kwenda nchi za ng’ambo, madai ambayo yalikanwa na chama hicho.
Chama cha KTDA kimelaumiwa vikali na seneta huyo kufuatia bei ya wakulima walipoongezwa mwaka jana ambayo ni ya pesa za ziada, na kusema kamati ya seneti kuhusu kilimo inaendelea kuangalia na kuchunguza mambo hayo kwa undani.
“Nitaufikisha mswada katika bunge la seneti kuhusu chama cha KTDA kujadiliwa na kupitishwa ili chama hicho kuwa chini ya uongozi wa serikali kuu ili kuzuia wizi ambao umekithiri na kushuhudiwa katika chama hicho,” alihoji Okong’o.
Wakati huo huo, seneta huyo alimtaka waziri wa kilimo Alex Kosgey kuchunguza kwa undani mambo yanayoendelea kutekelezwa katika chama hicho, ili wakulima waweze kujua na kubaini kama chama hicho kinajifaidhi chenyewe au kinawafaidi wakulima huku wakurugenzi wa viwanda wakiwa kati yao.
Kwa upande mwingine, wakulima wa viwanda mbalimbali kama Nyansiongo, Gianchore, miongoi mwa vingine wamelikumbatia ombi hilo la seneta Okong’o, kwani wanahitaji uwazi kutekelezwa katika viwanda hivyo.