Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o ameomba serikali kumchukulia katibu wa chama cha wazazi nchini Musau Ndunda hatua ya kisheria kwa kuwa kizuizi kwa uundaji wa bodi zitakazosimamimia shule za upili nchini.

Kulingana na Okong’o, chama cha Ndunda hakijulikani kisheria na hakuna haja ya Ndunda kuendelea kuingilia masuala ya elimu humu nchini.

Haya yanajiri baada ya kusemekana kuwa Ndunda anahitaji baadhi ya wanachama wake kuchaguliwa kwa mojawapo ya bodi za shule, jambo ambalo Okong’o alisema halitawezekana kamwe kwani ni kinyume na sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, Seneta Okong’o alisema anahitaji kujua kwa nini Musau Ndunda hajachukuliwa hatua ya kisheria hadi sasa baada ya kuingilia na kuzuia uundaji wa bodi za kusimamia shule za humu nchini.

Seneta huyo aliomba walimu wakuu wa shule kutomhusisha Ndunda kwa masuala ya elimu huku akisema kuwa hajulikani kisheria.

“Ndunda anastahili kuchukuliwa hatua kwani amekuwa kizuizi kwa uundaji wa bodi za kusimamia shule nchini,” alisema Okong’o.

Aliongeza ”Niliandikia wizara husika barua ya kusema kuwa Ndunda hajulikani kisheria na ninashangazwa kwa nini hajachukuliwa hatua hadi sasa.”