Seneta wa Nyamira Kennedy Mongare amelaani vikali kitendo cha maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi kuwakabili waandamanaji mjini Nairobi na Kisumu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumanne, Mongare alimtaka Inspekta Generali wa polisi Joseph Boinett kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa wa polisi waliomchapa mwandamanaji mmoja hadi akafa. 

"Maandamano ya jana ya wafuasi wa mlengo wa CORD yalikuwa ya amani na ni jambo la kushangaza kwamba maafisa wa polisi wanaostahili kulinda maisha ya wananchi wanaweza tumia nguvu kupita kiasa dhidi ya waandamanaji na ndio maana Inspecta Joseph Boinett sharti awachukulie hatua maafisa husika," alisema Mong'are.

Mong'are aliutaka muungano wa CORD kusitisha maandamano dhidi ya tume ya IEBC na kukumbatia majadiliano ya pamoja ili kusuluhisha tofauti baina ya muungano huo na tume ya IEBC. 

"Ombi langu kwa viongozi wa muungano wa CORD nikusitisha maandamano yanayoendelea dhidi ya tume ya IEBC kwa maana hatungependa tena kuona watu wetu wakiumizwa na maafisa wa polisi kama ilivyokuwa jana," aliongezea Mong'are.