Seneta wa Kaunti ya Nyamira ameunga mkono kongamano la vijana wa Kaunti la Nyamira linalotarajiwa kufanywa Desemba 27, 2015.
Akihutubia wakazi wa Nyansiongo alipotembelea eneo hilo siku ya Jumatatu, Seneta Kennedy Okong'o alisema kuwa amekuwa akifuatilia shughuli na miradi mbalimbali ya vijana, hali iliyomfanya kuunga mkono kongamano hilo la vijana.
"Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu miradi mbalimbali ya maendeleo ya vijana na nina furaha kujua kuwa sasa vijana wamefungua macho kwa kujihusisha na miradi ya maendeleo ili kupigania haki zao na kujiimarisha kiuchumi," alisema Okong'o.
Mongare aidha aliwahimiza vijana kuhakikisha kuwa wanaangazia masuala tata yanayo wakabili na kamwe wasiruhusu wanasiasa kuingililia kongamano hilo.
Aidha, aliwahimiza vijana kuandaa mapendekezo muhimu nakuyawasilisha kwa viongozi wakuu wa serikali ya kaunti ili kupata usaidizi.
"Nafahamu kuwa vijana wanaokongamana wanatoka kwenye milengo tofauti ya kisiasa na kwasababu hiyo, wanasiasa wanaopendelea sana kujipigia upatu wa kisiasa wanaweza tumia hafla hiyo ili kujiimarisha kisiasa. Nawaomba vijana kuhakikisha kuwa hawaruhusu hilo kutokea kwa kuhakikisha kuwa wanajadili tu changamoto zinazowakumba ili waandae mapendekezo nakuyawasilisha kwa viongozi wa serikali ya kaunti ili yaangaziwe," alisema Okong'o.