Seneta mteule Emma Mbura amewahimiza wakaazi Mombasa kujitenga na viongozi wachochezi ili kuepukana na mtafaruku wa kijamii.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Mombasa katika mkutano wa maendeleo ya wanawake siku ya Jumanne, Emma alisema kuwa tamaa ya uongozi na ubinafsi wa maendeleo nchini umepelekea viongozi wengi kukosa nidhamu na kuwachochea wananchi kuzua vurugu.

Mbura alisema kuwa ili kuepukana na mgawanyiko baina ya Wakenya kutokana na uchochezi wa kikabila, kisiasa na kidini, ni lazima kwa wakaazi kuwa katika mstari wa mbele kuhubiri amani na uiano nchini.

Seneta huyo alisisitiza Wakenya kuungana na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao ili kuwachagua viongozi waliowaadilifu.

“Tafadhali wananchi tujiepusha na hawa viongozi wasiojali maslahi yenu na wenye tamaa ya uongozi kwani wengi wao hupenda kuwachochea ili mvurugane ndio wao wafaidika kisiasa,” alisema Mbura.

Wakati huo huo, alitangaza kuwania kiti cha ubunge wa eneo la Rabai.

Alisema kuwa wakati umefika kwa wanawake kuchukua uongozi hadi mashinani.