Seneta mteule wa Kaunti ya Mombasa Emma Mbura amewapongeza wabunge wa ukanda wa Pwani kwa kutozua vurugu bungeni juma lililopita wakati Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa akilihutubia taifa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mbura aliitaja hatua ya wabunge wa upinzani kutoka Pwani kudinda kushirikiana na wenzao kuvuruga hotuba ya rais kama inayoashiria nidhamu waliyonayo wakaazi wa ukanda wa Pwani.
“Kila mtu aliona walivyofanya wabunge wa Cord. Wapwani tunajivunia kwa kuwa wabunge wetu hawakuwa miongoni mwao. Sisi ni watu wenye nidhamu na heshima. Pongezi kwa wenzetu kwa kudumisha heshima hiyo,” alisema Mbura.
Aidha, seneta huyo aliwasuta wabunge wa upinzani hasa wanaotoka magharibi mwa nchi kwa kile alichokitaja kama kutomheshimu Rais Kenyatta na kuwataka kutumia mbinu zingine kuikosoa serikali badala ya vurugu.
Siku ya Alhamisi juma lililopita, baadhi ya wabunge wa mrengo wa Cord walifurishwa bungeni baada ya kumzoa rais alipokuwa akilihutubia bunge kuhusiana na hatua ambayo taifa limepiga miaka mitatu tangu achaguliwe.