Kufuatia hali ambapo baadhi ya vijana walizua vurugu kwa kumzomea hadharani gavana wa kaunti ya Nyamira mbele ya rais kule Kebirigo wiki iliyopita, seneta wa kaunti hiyo amejitokeza kuwatetea vijana hao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiwahutubia wanahabari baada yake kuhudhuria hafla ya kuchangisha pesa kwenye kanisa la Kiadventista kule Kenyenya katika eneo bunge la Mugirango magharibi siku ya Jumamosi, Mong'are alisema kuwa wananchi wanaweza mzomea kiongozi yeyote iwapo hatekelezi majukumu yake inavyostahili.

“Unajua hawa wananchi ambao wametuajiri wanaweza wakamzomea kiongozi yeyote iwapo hatakelezi majukumu yake inavyostahili, na sioni iwapo vijana walikosea kumzomea gavana Nyagarama kwa maana serikali yake imefeli,” alisema Mong'are.

Mong'are aidha aliwashtumu vikali mawaziri wa serikali ya kaunti ya Nyamira kwa changamoto zinazoendelea kuikumba serikali ya kaunti hiyo.

“Ninalojua ni kwamba huenda gavana Nyagarama anatekeleza majukumu yake inavyostahili, ila baraza la mawaziri wake ndilo limefeli kwa kutotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo," aliongezea Mong'are.