Seneta mteule Emma Mbura ametangaza azma yake ya kuwania ubunge katika eneo bunge la Rabai mwaka wa 2017.
Mbura amesema kuwa imefikia wakati wa mabadiliko ambayo yamekuwa nadra kupatikana eneo hilo tangu mwaka wa 1963.
"Rabai inahitaji maendeleo kabambe haswa katika sekta ya elimu, kilimo na barabara. Mimi nitakuwa nikiomba kiti cha uwakilishi wa bunge la kitaifa hapa Rabai,” alisema Mbura.
Seneta huyo aliwarai wanawake kujihusisha kikamilifu na maswala ya kisiasa, huku akiongeza kuwa wakati wa wanawake kujitosa katika nyadhifa za uongozi ni sasa.
"Sekta ya kisiasa imetawaliwa na wanaume na imefikia wakati wa kuwadhibitishia kuwa sisi twaweza pia,” alisema Mbura.
Seneta huyo ana sifa kemkem kwa sababu ya kulitumia jina la aliyekuwa mpiganiaji wa uhuru kutoka jamii ya Giriama Mekatilili wa Menza.
Aliwasuta wanaompiga kulitumia jina hilo na kuwataka kutoingilia maswala hayo.
Seneta huyo analenga kumng'atua Mbunge wa Rabai William Kamoti ambaye alidai kuwa ameshindwa kutekeleza wajibu wake.