Kufuatia hatua ya gavana wa kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya kupuuza azma ya seneta wa Bungoma Moses Wetangula kuwania urais huku akiitaja hatua hiyo kama upigaji mbizi kwenye maji makuu, seneta wa kaunti ya Nyamira Okong'o Mong'are ameshtumu vikali hatua hiyo.
Kwenye mahojiano ya kipekee kwa njia ya simu siku ya Jumanne, Mong'are alisuta vikali matamshi ya Oparanya huku akiongeza kusema kuwa yafaa gavana huyo ampe heshima seneta Wetangula.
"Haya matamshi ya Gavana Oparanya kwamba seneta Wetangula hafai kuwania urais hayafai na hayana msingi kwa maana seneta Wetangula ni kiongozi wa kitaifa na yafaa aheshimiwe," alisema Mong'are.
Mong'are aidha aliongeza kwa kusema kwamba yafaa muungano wa CORD uchague kinara mmoja atakayewania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
"Ni sisitizo langu kwamba muungano wa CORD unastahili kumchagua mmoja kati ya vinara wa muungano ili kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, na hata kama kuna siasa za ni nani atakaye peperusha bendera kwenye muungano, ukweli ni kwamba tutaunga mkono yeyote atakayeteuliwa," aliongezea Mong'are.